Mustakabali wa Kiswahili kama Lugha ya Kufundishia Nchini Tanzania: Uhakiki wa Maudhui ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014
Year: 2017
Type: article
Abstract: Msingi wa makala haya ni “Sera ya Elimu na Mafunzo” (SEM, 2014). Makala yanahakiki nafasi ya lugha ya Kiswahili kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo nchini Tanzania na mustakabali wake kwenye mfumo wa elimu kama lugha ya kufundishia. Mbinu iliyotumika ni ya maktabani ambapo mwandishi alisoma na kuhakiki maudhui ya SEM msisitizo ukiwa kwenye masuala yahusuyo lugha ya kufundishia. Uchambuzi wa kiisimujamii ulitumika ili kuonesha ukinzani baina ya matamko ya SEM. Tamko la SEM kuhusu lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia haliakisi hali halisi. Uhusiano wa Kiisimujamii wa lugha ya Kiswahili na ya Kiingereza kuhusu elimu unatoa tafsiri kuwa endapo SEM itatumika bila nia ya dhati ya kuisaidia lugha ya Kiswahili basi lugha hiyo inaweza kutoweka kabisa kwenye mfumo wa elimu kama lugha ya kufundishia. Makala yanajenga hoja kuwa tamko la SEM kwamba Kiingereza na Kiswahili ziwe na hadhi sawa kwenye mfumo wa elimu linatia moyo kwa mustakabali wa lugha ya Kiswahili lakini utekelezaji wake unaibua changamoto nyingi kwa namna ambayo zisipotazamwa kwa makini lugha ya Kiingereza itaendelea kukita mizizi zaidi na kujenga uwezekano wa jamii kukataa kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu mwelekeo wa jamii unanasibisha elimu na Kiingereza. Mwisho, wito unatolewa kwa watunga sera kusitisha kutumia lugha ya wachache kutoa elimu kwa wengi kwa kuwa kufanya hivyo ni kubadili malengo ya elimu.
Author: Gervas Kawonga
Language: Swahili
Subfield: Linguistics and Language
Field: Social Sciences
Domain: Social Sciences
SDG: Quality education
Open Access status: bronze
OpenAlex ID: W3034896268
