Miangwi ya Mazingira ya Mwandishi katika Utunzi wa Riwaya za Kimwingilianomatini Kimpito-Wakati: Mfano wa Utengano na Kidagaa Kimemwozea
Year: 2026
Type: article
Abstract: Kwa kurejelea riwaya ya Utengano (1980) yake Said A. Mohamed na Kidagaa Kimemwozea (2012) ya Ken Walibora, makala hii inahakiki jinsi mazingira ya waandishi yanavyoathiri utunzi wa riwaya za kimwingilianomatini kimpito-wakati. Hoja ijengwayo ni kwamba mazingira ya kiuchumi, kisiasa, kitamaduni, na ya kiasili yawazungukayo waandishi yana dhima katika mwingiliano na uendelezaji wa maudhui na fani kupitia vizazi viwili tofauti vya wanariwaya. Kwa mwongozo wa nadharia ya Mwingilianomatini iliyoasisiwa na Julia Kristeva, makala hii imekitwa katika muundo wa kiuchanganuzi. Uchunguzi huu uliofanywa maktabani unayatamba mawanda ya mwingilianomatini kwa kuchambua athari za mazingira ya waandishi katika utuzi wa riwaya zao kimpito-wakati. Wango la utafiti linajumuisha riwaya za Kiswahili 12 zinazoakisi mwingilianomatini na ambazo zilichapishwa kati ya 1980 na 2012. Hata hivyo, usampulishaji lengwa ndio uliotumika kuteua mbili tu - Utengano na Kidagaa Kimemwozea. Data msingi zilikusanywa kwa usomaji wa kina wa riwaya teule, nazo data za upili zikapatikana kutoka kwa vitabu, tasnifu, makala na machapisho mengine ya kitaaluma. Data ya kitaamuli iliyokusanywa ilichanganuliwa kithamano kwa mwongozo wa mihimili ya nadharia ya Mwingilianomatini na kuwasilishwa kwa maelezo. Matokeo ya utafiti yanadhihirisha kuwa mazingira duni ya kisiasa ya baada ya uhuru, ukandamizaji wa kijinsia, na usomi wa waandishi uliuchochea mwangwi wa kimpito-wakati uliopo kati ya matini ya Walibora inayozungumza na kuikuza matini ya Mohamed. Utafiti unahitimisha kuwa ingawa Ken Walibora na S.A. Mohamed walikulia katika maeneo, nyakati na tamaduni zisizofanana, wameathiriwa na mazingira yao ya kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na kidini kwa njia zinazofanana..
Language: Swahili
Subfield: Literature and Literary Theory
Field: Arts and Humanities
Domain: Social Sciences
Open Access status: diamond
OpenAlex ID: W7208829434
